Bayer Kuzindua Kampeni ya Kuwahamasisha Wakulima Kuhakiki Mbegu Halisi
- Exview Communications
- 11 hours ago
- 2 min read

Kampeni inayolenga kuwahamasisha wakulima kuhusu umuhimu wa kuthibitisha mbegu halisi kabla ya kupanda itazinduliwa kesho mjini Mwanza.
Kampeni hiyo, iliyopewa jina la “DEKALB Mafanikio Shambani,” itazinduliwa na kampuni ya Bayer East Africa kwa ushirikiano na Wizara ya Kilimo pamoja na wadau wa sekta ya mbegu nchini, ikiwa na lengo la kuwasaidia wakulima wa mahindi kuongeza tija na kuimarisha usalama wa chakula nchini.
Aidha, uzinduzi huo utahusisha promosheni ya miezi minne itakayowazawadia wakulima watakaoshiriki kwa kufuata utaratibu wa uthibitishaji wa mbegu.
Kampeni hiyo ya kitaifa itawalenga wakulima wa mahindi nchini Tanzania na itahusisha aina tano za mbegu chotara za mahindi za DEKALB. Aina hizo za mbegu zimezalishwa kwa kuzingatia mazingira tofauti ya kilimo, yakiwemo maeneo yenye kiwango kidogo cha mvua pamoja na maeneo yenye uwezo mkubwa wa uzalishaji, ili kuwasaidia wakulima kupata mavuno yenye uhakika licha ya mabadiliko ya hali ya hewa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bayer East Africa, John Kanyingi, amesema athari za mabadiliko ya tabianchi zimeendelea kuwa changamoto kwa wakulima wadogo katika ukanda huu, hali inayoongeza umuhimu wa matumizi ya aina za mbegu za mahindi zinazoweza kuongeza uzalishaji na ustahimilivu.
“Wakulima wadogo ndio wanaoathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi na hali ya hewa isiyotabirika barani Afrika. Kama kampuni inayotambua usalama wa chakula kuwa sehemu muhimu ya usalama wa taifa, tunahamasisha matumizi ya mbegu zilizothibitishwa ambazo zinaweza kuwasaidia wakulima kuongeza mavuno huku zikichangia kilimo endelevu,” amesema Kanyingi.
Katika kipindi cha miezi minne ya promosheni hiyo, wakulima watakaoshiriki watapata nafasi ya kujishindia zawadi mbalimbali zikiwemo pampu za kunyunyizia dawa za mgongoni, simu janja, mashine za kupandia mahindi zinazoendeshwa kwa mkono, pikipiki, paneli za sola na mashine za kukoboa mahindi. Wakulima wawili watajishindia magari mawili aina ya Toyota pick-up.
Ili kushiriki, mkulima anatakiwa kununua mbegu kutoka kwa wauzaji wa pembejeo walioidhinishwa katika eneo lake, kisha kukwangua kibandiko cha uthibitishaji wa kielektroniki cha TOSCI ili kupata namba ya siri.
Baada ya hapo, mkulima atapiga 14852# na kuingiza namba hiyo yenye tarakimu 12. Atapokea ujumbe mfupi wa kuthibitisha ushiriki wake na kuingizwa kwenye droo ya promosheni.
“Tunawasaidia wakulima kulinda mavuno yao kwa kuhakikisha wanathibitisha uhalisi wa mbegu kabla ya kupanda, huku tukitoa motisha inayolenga kuimarisha usalama wa chakula,” ameongeza Kanyingi.
Washindi wa promosheni hiyo watatangazwa kila baada ya wiki mbili. Katika kipindi cha miezi minne ya kampeni, Bayer itaendelea kuwafikia wakulima kwa mbegu bora pamoja na suluhisho nyingine za kilimo katika juhudi za kuendeleza uzalishaji endelevu wa chakula nchini.
.png)



Comments